N/AºC, Unavailable
Tuesday, 15th July, 2025
Posted: 2025-02-19
Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Shamata Shaame Khamis, ameeleza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha ulinzi katika misitu ya hifadhi ili isipoteze uhalisia wake lakini kuongeza kasi ya maendeleo ya sekta za Kilimo na Utalii. Shamata alieleza hayo wakati wa Ugawaji wa sare za kazi kwa wafanyakazi wa kitengo cha uhifadhi wa msitu wa Kiwengwa Pongwe, wilaya wa Kaskazini ‘B’, mkoa wa Kaskazini Unguja. Amesema hatua hiyo imetokana na azma ya Wizara kuimarisha mashirikiano na Mwekezaji kutoka katika kampuni ya Michel Mantheakis Safari Zanzibar Ltd kutekeleza shughuli mbali mbali za ulinzi na uendelezaji wa msitu huo. Hata hivyo Shamata aliwasisitiza wafanyakazi hao kuvaa sare hizo wanapokuwa kazini Kwani zitaweza kuwarahisishia wananchi na watalii wanaotembelea eneo hilo kutofautisha baina ya walinzi na watembezaji wageni sambamba na kuimarisha ulinzi katika maeneo ya hifadhi. Aidha amesema Serikali haitosita kuwachukulia hatua za kisheria wanaofanya uharibifu katika msitu huo kutokana na shughuli wanazozifanya katika msitu zitakazopelekea kuharibu mazingira na kutoweka kwa maliasili zinazopatikana ndani ya msitu huo. "Ninawaomba wananchi waache mara moja uharibifu wa mazingira kwani hatutakuwa na muhali wala kumuonea huruma mtu yeyote atakayebainika kufanya uharibifu wa mazingira katika hifadhi za misitu na hatua za kisheria zitachukuliwa juu yake", amesema Shamata. Amesema kumejitokeza uvamizi wa msitu huo kwa shughuli za kibinadamu zikiwemo za kilimo, ujenzi, ukataji wa miti kiholela, uchomaji moto katika hifadhi ya msitu jambo ambalo litakalopelekea kupoteza haiba na uhalisia wa mazingira. "Serikali yetu inategemea rasilimali misitu kwa sababu ikitunzwa vizuri itapelekea kupatikana kwa mazingira mazuri, hewa safi, maji safi, kuongezeka kwa idadi ya watalii na uwiano wa viumbe hai hivyo ni wajibu wetu kutunza hifadhi zetu ili tuweze kukusanya mapato kwa ajili yetu na taifa kwa ujumla", amefahamisha Shamata. Kwa upande wake Meneja wa Mradi wa uhifadhi wa msitu huo Said Hassan Mnkeni, amesema lengo la mradi huo ni kuanzisha uwindaji wa kitalii wa paa nunga ili kuongeza idadi ya paa katika hifadhi na kuinua pato la Serikali. Pia Said amewasisitiza, wafanyakazi kushirikiana na jamii inayozunguka msitu huo kwa kuwapatia elimu ili waachane na tabia ya uharibifu wa mazingira . Kwa upande wake Naibu Sheha wa Kiwengwa Pongwe, Vuai Ame Kombo, amesema wataishauri jamii kuzingatia uhifadhi wa rasilimali za msitu huo ili zibaki salama na kuepuka kufanya uvamizi wa kuharibu maliasili zinazopatikana kwenye msitu huo. Aidha amewasihi wanajamii kuachana na dhana potofu za kuharibu maliasili zilizowazunguka kwani ni chanzo cha kuinua uchumi na taifa pamoja na Upatikanaji wa ajira kuptia msitu huo. Mapema Msaidizi Mkuu wa hifadhi hiyo, Mohamed Kombo Khatib akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wenziwe ameeleza kufurahishwa kwao kutokana na kupatiwa sare hizo kwani zitawasaidia kuimarisha ulinzi na kuaminika kwa wanajamii wanaoizunguka hifadhi ya msitu huo. Msitu wa Kiwengwa Pongwe una ukubwa wa kilomita za mraba 33 sawa na hekta 3,332 na umezungukwa na vijiji 13 ukiwa na jumla ya wafanyakazi 20 waliopatiwa sare hizo zilizogharimu shilingi milioni 4.2.
Fans
Followers
Followers
Subscribers