- Total Visitors: 12,428
Tuesday, 21st October, 2025
Posted: 2025-10-15
NA SALAMA MOHAMED, WKUMM. AFISA Kiungo katika Kitengo cha Elimu kwa Wakulima Zanzibar kupitia Mradi wa Uhimilivu wa Mifumo ya Chakula Tanzania Zanzibar, Fatma Himid Ali, ameeleza kuwa ziara ya Mabibi na Mabwana shamba wa Unguja na Pemba mkoani Morogoro imelenga kujifunza matumizi ya teknolojia za kisasa za kilimo kuongeza zao la uzalishaji na ubora wa mazao visiwani. Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Fatma alieleza wataalamu hao pia wataweza kubadilishana uzoefu na kuona mafanikio ya watafiti wa taasisi za kilimo mkoani humo wakiwemo wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kituo cha Dakawa. "Kuna umuhimu wa kujifunza teknolojia mbali mbali za kilimo ili kuongeza tija na mafanikio katika uzalishaji. Tunataka washiriki hawa wakirudi Zanzibar wawe mabalozi wa mabadiliko ya kilimo cha kisasa”, alisema Fatma. Akiwa na timu ya wataalamu hao katika shamba la mbegu za nafaka la TARI Dakawa, wilaya ya Mvomero, Morogoro, Fatma alisema maarifa watakayoyapata yatawasaidia wakulima kuongeza tija na kuimarisha ubora wa mazao, sambamba na kuimarisha mfumo wa chakula katika visiwa vya Zanzibar. Kwa upande wake, Mkurugenzi wa TARI kituo cha Dakawa, Jerome Jonathan Mghase, alisema kituo hicho kilianzishwa mwaka 1984 kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Korea na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kikilenga kuzalisha mbegu bora za nafaka, matunda na mboga mboga, pamoja na kusambaza teknolojia bunifu za kilimo kwa wakulima. "Tunatoa teknolojia zinazolenga kuongeza tija, kupunguza gharama za uzalishaji na kuhakikisha mkulima anapata mazao yenye ubora yanayokidhi soko la ndani na nje”, alisema Mghase. Nae Bibi Shamba wa wilaya ya Kusini Pemba, Subira Ame Silima, alisema ziara hiyo imekuwa na manufaa makubwa kwani imewapa uelewa mpya kuhusu mbinu shirikishi za kilimo, ikiwemo mchanganyiko wa mazao kama migomba na nyanya chungu, unaosaidia kuongeza kipato cha mkulima. "Tumepata ujuzi wa vitendo na tumeona njia mbalimbali za kuongeza tija bila kutumia gharama kubwa. Tunaomba Serikali iendelee kutoa hamasa na mafunzo kama haya mara kwa mara”, alisema Subira. Ziara hiyo iliyoanza juzi imehusisha wataalamu wa kilimo 31 wa Unguja na Pemba, waliotoka katika Idara ya Umwagiliaji Maji, Idara ya Kilimo na Uhakika wa Chakula za Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa Uhimilivu wa Mifumo ya Chakula Tanzania Zanzibar. Wakati wa ziara hiyo, washiriki hao walitembelea TARI kitoa cha Dakawa, viwanja vya nane nane na vituo vya utafiti wa kilimo kwa lengo la kujifunza teknolojia mpya na kubadilishana uzoefu utakaosaidia kuendeleza sekta ya kilimo Zanzibar.
\r\nFans
Followers
Followers
Subscribers