Event Details
Photo

Posted: 2025-02-23

Ufunguzi wa Mradi wa Usimamizi wa Hifadhi ya Akiba ya Ufufuma-Pongwe Kuleta Manufaa kwa Misitu na Wanyamapori.

Description

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Ali Khamis Juma, amesema kuwa kuwepo kwa Hifadhi ya Akiba ya Ufufuma-Pongwe kutaleta manufaa makubwa kwa bioanuwai ya misitu na wanyamapori, pamoja na jamii inayozunguka Hifadhi ya Kiwengwa-Pongwe.

Aliyasema hayo wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Usimamizi wa Hifadhi ya Akiba ya Ufufuma-Pongwe, uliofanyika katika Ofisi za Wizara ya Kilimo, Maruhubi, Wilaya ya Magharibi A, Unguja.

Amesema hifadhi hiyo ni eneo muhimu linalounganisha maeneo mbalimbali yanayotumiwa na wanyamapori kwa ajili ya kutafuta chakula, maji, kuzaliana, kukimbia maadui, na kukwepa majanga ya kiasili na yale yanayosababishwa na binadamu.

Aidha, ameeleza kuwa Idara ya Misitu, kwa kushirikiana na Jumuiya ya Uhifadhi wa Wanyamapori na Mimea (WCS) Tanzania, inatekeleza mradi huo kwa lengo la kuzuia uharibifu wa misitu, kuimarisha makazi ya wanyamapori, na kushirikisha jamii katika juhudi za uhifadhi.

Hifadhi hiyo ina jumla ya hekta 1,988 na imezungukwa na Shehia nane, ambazo ni Marumbi, Jendele, Bambi, Chwaka, Uroa, Pagali, Umbuji, na Pongwe.

Akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uhifadhi wa Wanyamapori na Mimea Tanzania (WCS), Afisa Muendeshaji wa Mradi Zanzibar, Said Abdallah Fakih, amesema kuwa mradi huo wa mwaka mmoja unatarajiwa kuanza tarehe 25 Februari mwaka huu, ambapo jumla ya shilingi 115,200,000 zitatumika kwa shughuli za uendeshaji wa mradi huo.

Aidha, amebainisha kuwa mradi huu unalenga kulinda na kuhifadhi wanyamapori adimu na wa kipekee ili kuhakikisha wanaendelea kuwepo kwa manufaa ya mazingira na vizazi vijavyo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Sheha wa Shehia ya Pongwe, Fatma Vuai Faki, amesema kuwa hifadhi hiyo italeta faida kubwa kwa kurejesha misitu ya asili na kusaidia wanyama kuendelea kuwepo.

Hata hivyo, ameomba serikali kuimarisha ulinzi wa maeneo ya hifadhi ili jamii iweze kufurahia rasilimali za wanyama ambao hupatikana Zanzibar pekee.

Follow Us