Event Details
Photo

Posted: 2025-02-21

Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Shamata Shaame Khamis, ameeleza kuwa Serikali itaendelea......

Description

Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Shamata Shaame Khamis, ameeleza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha ulinzi katika misitu ya hifadhi ili isipoteze uhalisia wake lakini kuongeza kasi ya maendeleo ya sekta za Kilimo na Utalii.

Shamata alieleza hayo wakati wa Ugawaji wa sare za kazi kwa wafanyakazi wa kitengo cha uhifadhi wa msitu wa Kiwengwa Pongwe, wilaya wa Kaskazini ‘B’, mkoa wa Kaskazini Unguja.

Amesema hatua hiyo imetokana na azma ya Wizara kuimarisha mashirikiano na Mwekezaji kutoka katika kampuni ya Michel Mantheakis Safari Zanzibar Ltd kutekeleza shughuli mbali mbali za ulinzi na uendelezaji wa msitu huo.

Hata hivyo Shamata aliwasisitiza wafanyakazi hao kuvaa sare hizo wanapokuwa kazini Kwani zitaweza kuwarahisishia wananchi na watalii wanaotembelea eneo hilo kutofautisha baina ya walinzi na watembezaji wageni sambamba na kuimarisha ulinzi katika maeneo ya hifadhi.

Aidha amesema Serikali haitosita kuwachukulia hatua za kisheria wanaofanya uharibifu katika msitu huo kutokana na shughuli wanazozifanya katika msitu zitakazopelekea kuharibu mazingira na kutoweka kwa maliasili zinazopatikana ndani ya msitu huo.

"Ninawaomba wananchi waache mara moja uharibifu wa mazingira kwani hatutakuwa na muhali wala kumuonea huruma mtu yeyote atakayebainika kufanya uharibifu wa mazingira katika hifadhi za misitu na hatua za kisheria zitachukuliwa juu yake", amesema Shamata.

Amesema kumejitokeza uvamizi wa msitu huo kwa shughuli za kibinadamu zikiwemo za kilimo, ujenzi, ukataji wa miti kiholela, uchomaji moto katika hifadhi ya msitu jambo ambalo litakalopelekea kupoteza haiba na uhalisia wa mazingira.

"Serikali yetu inategemea rasilimali misitu kwa sababu ikitunzwa vizuri itapelekea kupatikana kwa mazingira mazuri, hewa safi, maji safi, kuongezeka kwa idadi ya watalii na uwiano wa viumbe hai hivyo ni wajibu wetu kutunza hifadhi zetu ili tuweze kukusanya mapato kwa ajili yetu na taifa kwa ujumla", amefahamisha Shamata

Follow Us