N/AºC, Unavailable
Sunday, 31st August, 2025
Posted: 2025-08-16
Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar imesema itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuimarisha sekta ya kilimo nchini, hasa katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.\r\n\r\nKauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Ali Khamis Juma, wakati wa uzinduzi wa mradi Kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi uliofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Kilimo, Maruhubi.\r\n\r\nAmesema Mradi huo unalenga kupunguza upungufu wa uzalishaji wa chakula unaosababishwa na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi, kwa kuboresha mbinu za kilimo, hususan kilimo cha mpunga.\r\n\r\nAkizungumza katika hafla hiyo, Katibu Mkuu amesema kuwa mafanikio ya mradi huo yatabadilisha mtazamo wa wakulima kuhusu kilimo, na kusaidia kuongeza upatikanaji wa chakula cha uhakika katika misimu yote ya mavuno, hivyo kuondoa utegemezi wa chakula kutoka nje ya nchi.\r\n\r\nAidha, amesema kuwa kila mdau anawajibu wa kusimamia kwa umakini utekelezaji wa mradi huo, ili kuhakikisha uzalishaji unaongezeka na taifa linaondokana na changamoto ya uhaba wa chakula.\r\n\r\nAmesema Serikali ina imani kuwa mradi huo utaongeza tija katika kilimo, kuboresha uhifadhi wa mazao kupitia ujenzi wa maghala ya kisasa, na hivyo kuwa na akiba ya chakula wakati wote.\r\n\r\nPia, ameeleza kuwa serikali ina mpango wa kuanzisha kilimo cha biashara kwa mazao mbali na mpunga, ili kuongeza fursa za kiuchumi na kujenga kilimo chenye tija ndani na nje ya nchi.\r\n\r\nKupitia utafiti huo, serikali inatarajia kupambana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi kwa kuchagua mbegu bora zitakazotoa mavuno mengi katika mazingira magumu, pamoja na kutengeneza aina mpya ya mbolea inayohifadhi unyevu na kuongeza virutubisho vya udongo.\r\n\r\nAidha, Katibu ameongeza kuwa serikali haitasita kuchukua hatua dhidi ya mtu yeyote atakayekiuka makubaliano ya utekelezaji wa mradi huo. Hata hivyo, amesema changamoto ya uhaba wa bajeti za utafiti imepata afueni kupitia ufadhili wa mradi huo.\r\n\r\nKwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo na Mifugo Zanzibar, Abdallah Ibrahim Ali amesema mradi huo pia unalenga kuzalisha mbegu himilivu za mpunga dhidi ya ukame na chumvi, sambamba na kuzalisha majani ya mifugo yenye virutubisho kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa maziwa bora.\r\n\r\nNaye, Afisa Uratibu wa Utafiti kutoka Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Dr Kurwa Kangata, amesema mradi huo unalenga kutoa suluhisho la muda mrefu kwa changamoto za kilimo, na kusisitiza umuhimu wa utekelezaji kwa wakati na kwa kuzingatia ubora.\r\n\r\nAmesisitiza pia umuhimu wa kuwasilisha ripoti za utekelezaji wa mradi ili kutoa mrejesho wa maendeleo na mafanikio ya mradi huo baada ya kukamilika.\r\n\r\nUzinduzi wa mradi huo umehudhuriwa na wakuu wa wilaya, maafisa kutoka Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, maafisa kilimo wa wilaya, wataalamu kutoka Tume ya Sayansi na Teknolojia ya Tanzania Bara na Zanzibar, pamoja na wakulima kutoka maeneo mbalimbali.