N/AºC, Unavailable
Sunday, 31st August, 2025
Posted: 2025-08-14
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Ali Khamis Juma, amesema kuwa misitu ni miongoni mwa vyanzo vikuu vya uhai kwa binadamu, hivyo ni muhimu kuitunza, kuihifadhi na kuepuka uharibifu wake ili iweze kuendelea kuwa na faida kwa jamii na taifa kwa ujumla.\r\n\r\nAkizungumza katika mahojiano maalum kwenye kipindi cha Asubuhi Njema kilichorushwa na ZBC TV, Katibu Mkuu alitoa kauli hiyo wakati akiwa katika banda la Idara ya Misitu kwenye Viwanja vya Maonesho ya Wakulima (Nane Nane) vilivyopo Dole Kizimbani, Wilaya ya Magharibi \'A\', Unguja.\r\n\r\n\"Iwapo tutaharibu misitu, tunaharibu uhai wetu. Hatutapata mvua kama hakuna misitu, hatuwezi kupata chakula bila misitu. Hivyo, ni wajibu wa kila mmoja wetu kuhakikisha tunaitunza misitu kwa ajili ya maisha yetu na vizazi vijavyo,\" alisema Katibu huyo.\r\n\r\nAli Khamis aliongeza kuwa ni faraja kubwa kuona jamii inaendelea kuonyesha mshikamano katika utunzaji wa rasilimali za misitu, kwani huchangia katika pato la taifa na ulinzi wa mazingira.\r\n\r\nKatika kuonyesha umuhimu wa sekta ya misitu, Katibu Mkuu alieleza kuwa Wizara imejipanga kutoa elimu kwa wananchi kupitia maonesho hayo, kwa kuonyesha miti ya aina mbalimbali ikiwemo ya chakula, miti ya asili ya misitu, pamoja na wanyama wanaotegemea mazingira ya misitu ili vijana na jamii kwa ujumla waweze kujifunza na kushiriki kikamilifu katika utunzaji wa mazingira.\r\n\r\n\"Tumekuwa tukiweka miti ya aina tofauti katika maonesho haya, si tu kwa ajili ya urembo bali kwa elimu na hamasa hivyo uwepo wa wanyama mbalimbali huwavutia vijana na kuwajengea uelewa wa umuhimu wa misitu,\" aliongeza.\r\n\r\nKwa upande wake, Mratibu wa Maonesho hayo, Ruzuna Rajab, alisema mwaka huu maonesho yamepata mwitikio mkubwa kutokana na ongezeko la washiriki kutoka Tanzania Bara na hata kutoka nje ya nchi, huku taasisi nyingi zikiwasilisha ubunifu na huduma zao kwa jamii.\r\n\r\n\"Kila mmoja ni shahidi wa mafanikio ya maonesho haya. Wananchi wamejitokeza kwa wingi wengine kwa ajili ya kujifunza na wengine kwa matembezi ya kawaida lakini ujumla wake ni kwamba hamasa imekuwa kubwa mno mwaka huu,\" alisema Ruzuna.\r\n\r\nAidha, ameiomba serikali kupitia taasisi husika kuangalia namna ya kuboresha miundombinu ya eneo hilo kwa kulifanya kuwa la kudumu, ikiwa ni pamoja na kujenga majengo ya kisasa na kuweka huduma muhimu kwa ajili ya maonesho yajayo.\r\n\r\nMaonesho ya Wakulima Nane Nane Zanzibar yalianza rasmi tarehe 1 Agosti na yanatarajiwa kufikia kilele chake tarehe 14 Agosti mwaka huu, yakibeba kaulimbiu isemayo: \"Kilimo ni Utajiri, Tunza Amani, Lima Kibunifu.\"