N/AºC, Unavailable
Wednesday, 17th September, 2025
Posted: 2025-09-12
Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Shamata Shaame Khamis, amelaani vikali kitendo cha wizi wa transfoma mbili zenye thamani ya shilingi milioni 28 kilichofanywa na watu wasiojulikana katika maeneo ya mabonde ya Umwagiliaji huko Cheju, Wilaya ya Kati Unguja. Akizungumza mara baada ya kutembelea eneo hilo la tukio, Waziri Shamata alisema kuwa transfoma hizo zilikuwa na uwezo wa kuendesha visima viwili vya maji kwa ajili ya kumwagilia mashamba, na kwamba tukio hilo limeathiri zaidi ya wakulima 1,000 ambao sasa wamesitisha shughuli za kilimo kutokana na ukosefu wa huduma ya umwagiliaji. \"Haiwezekani Serikali iwekeze fedha nyingi kwa ajili ya maendeleo ya kilimo halafu watu wachache waibuke na kufanya uharibifu wa aina hii. Matendo haya yanarudisha nyuma juhudi za Serikali na wananchi,” alisema Waziri Shamata. Waziri huyo aliongeza kuwa Wizara yake kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kati, itaendelea kufuatilia tukio hilo hadi wahusika watakapokamatwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria. Aidha, alitoa wito kwa viongozi wa kamati ya wakulima katika bonde hilo kuendelea kushirikiana na Serikali, kuwa wavumilivu, huku Serikali ikitafuta suluhisho la haraka ili kurejesha huduma za umwagiliaji na kuendelea na shughuli za uzalishaji. Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kati, Rajab Ali Rajab, alisema wizi huo umeleta athari kubwa kwa wakulima waliokuwa katika kipindi muhimu cha kupanda mpunga. Alisema kukosekana kwa maji kumesababisha wakulima kusitisha shughuli zao za kilimo. \"Kesi ya tukio hili tayari imefunguliwa katika kituo cha Polisi Tunguu, na vyombo vya ulinzi na usalama vimeanza uchunguzi ili kuwabaini waliohusika,” alisema Mkuu huyo wa Wilaya. Rajab alitoa wito kwa wananchi na taasisi mbalimbali kushirikiana kulinda miundombinu ya umwagiliaji kama transfoma hizo, akisisitiza kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha wakulima wanalima kwa tija na kupata mavuno bora bila kuiweka Serikali kwenye gharama zisizo za lazima. \"Ni ukweli usiopingika kwamba matukio kama haya yanarudisha nyuma maendeleo ya nchi. Serikali inafanya kazi kubwa ya kuleta maendeleo, lakini tukiruhusu uharibifu wa aina hii, tunajikosesha fursa za maendeleo,” aliongeza. Naye Katibu wa Bonde la Cheju, Kassim Suleiman Mdunga, alieleza kuwa tukio hilo limewarudisha nyuma wakulima kwa kiasi kikubwa. Alitoa wito kwa wananchi kuacha kuhujumu mali za Serikali na kusisitiza kuwa hatua za kuimarisha ulinzi kwenye maeneo hayo zimeanza kuchukuliwa ili kuzuia matukio kama hayo kujirudia. Transfoma zilizoibiwa zina ukubwa wa KVA 100 kwa kila moja na kwa jumla zinatumika kuendeshea pampu 4 za maji zinazotumika kwa shughuli za umwagiliaji kwenye mabonde hayo.
Fans
Followers
Followers
Subscribers