Posted: 2026-04-03
Naibu Waziri Dkt. Salum Soud Hamed, Aonya Dhidi ya Ujenzi Kinyume na Makubaliano ya Mradi Kisakasaka
Article Details
Naibu Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Mhe. Dkt. Salum Soud Hamed amesema Wizara haijaridhishwa na maendeleo ya ujenzi unaoendelea katika eneo la Kisakasaka, unaohusisha miundombinu ya kuingilia mifugo bandarini pamoja na josho la kuoshea mifugo.
\r\nAkizungumza mara baada ya kufanya ziara ya ukaguzi katika eneo hilo, Mhe. Dkt. Hamed ameeleza kuwa kuna tofauti kati ya makubaliano ya awali yaliyopo kwenye michoro ya mradi na hali halisi ya ujenzi unaoendelea. Amesisitiza kuwa hali hiyo haiwezi kuvumilika, hasa ikizingatiwa umuhimu wa mradi huo katika kuimarisha sekta ya mifugo Zanzibar. Amebainisha kuwa moja ya kasoro zilizobainika ni uwepo wa miundombinu ya uzio wa kuhifadhia mifugo baada ya kutoka katika josho, ambayo imejengwa kinyume na makubaliano ya kitaalamu yaliyowekwa. Awali, Msimamizi wa Mradi kutoka Wakala wa Majengo Zanzibar (ZBA), Bw. Nasor Mohamed Hamad, amekiri kuwepo kwa changamoto katika utekelezaji wa mradi huo na kuahidi kuzifanyia kazi kwa haraka ili kuhakikisha ujenzi unazingatia viwango na makubaliano yaliyowekwa. Ameeleza kuwa hadi sasa, ujenzi umefikia asilimia 70 na hatua za ukamilishaji zinaendelea.
\r\nMradi huo wa ujenzi na uboreshaji wa machinjio pamoja na eneo la kuingilia na kuhifadhia mifugo kwa upande wa Unguja-Kisakasaka na Pemba- Nzi wengi, umegharimu jumla ya shilingi bilioni 2.3, ambapo hadi sasa kiasi cha shilingi bilioni 1.3 kimeshalipwa kwa mkandarasi kwa ajili ya utekelezaji wa kazi hiyo. Wizara imesisitiza umuhimu wa usimamizi makini wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana na malengo yaliyokusudiwa yanafikiwa kwa wakati.

