Posted: 2026-02-12
WAZIRI MAKAME AZINDUA ZOEZI LA CHANJO YA KICHAA CHA MBWA
Article Details
Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Mhe. Suleiman Masoud Makame, amezindua rasmi zoezi la utoaji wa chanjo ya ugonjwa wa kichaa cha mbwa lililofanyika katika eneo la Mseweni, Wilaya ya Kati Unguja. Uzinduzi wa zoezi hilo umehudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Kati Unguja, Mhe. Rajab Ali Rajab, pamoja na Madaktari wa Mifugo, Maafisa Mifugo, wafugaji na wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo. Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Makame amesema zoezi la chanjo lina lengo la kudhibiti na hatimaye kutokomeza kabisa ugonjwa wa kichaa cha mbwa, ambao ni hatari kwa afya na maisha ya binadamu pamoja na wanyama. Ameeleza kuwa zoezi hilo ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya kulinda afya ya jamii na mifugo kwa ujumla. Ameongeza kuwa utoaji wa chanjo umeleta mafanikio makubwa, ambapo Wilaya ya Kati Unguja imefanikiwa kufikia asilimia 70 ya chanjo, na hakuna tukio lolote lililoripotiwa la ugonjwa wa kichaa cha mbwa kwa binadamu wala wanyama katika kipindi cha hivi karibuni.
\r\n\r\n" muelekeo wa Serikali ni kuutokomeza kabisa ugonjwa huo nchini" amesema Suleiman
\r\n\r\nKwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Mifugo, Bi. Asha Zaharan Mohamed, amesema zoezi hilo hufanyika kila mwaka na muonekano ni kupunguwa kwa kiasi kikubwa kwa maambukizi na ugonjwa wa kichaa cha mbwa kuwa miongoni mwa magonjwa yanayoambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu. Ameeleza kuwa Zanzibar ina jumla ya mbwa takribani 8,000 katika visiwa vya Unguja na Pemba, ambapo Wilaya ya Kati Unguja ina mbwa 1,228, amehimiza ushirikiano wa jamii na wafugaji katika kuhakikisha mbwa wote wanapatiwa chanjo ili kuwalinda dhidi ya maambukizi na kulinda usalama wa jamii kwa ujumla. Akitoa shukrani kwa Serikali, mmoja wa wafugaji, Mohamed Mahamud Omar, amesema kwa sasa hakuna matukio ya watu kutafunwa na mbwa, jambo linaloonesha juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali katika kuleta madaktari wa mifugo na kutoa chanjo. Amewataka wafugaji wenzake kujitokeza kwa wingi kuwapatiwa mbwa wao chanjo kwa usalama wa mifugo yao na jamii.
\r\n

