- Total Visitors: 111,778
Friday, 23rd January, 2026
Posted: 2026-01-05
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo imeahidi kuendelea kuwasaidia wakulima wa zao la mpunga pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili ili kuongeza uzalishaji na kipato chao.
\r\n\r\nKauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Saleh Mohamed Juma, wakati akifungua kikao cha kujadili changamoto za Kituo cha Kilimo cha Bonde la Kibonde Mzungu pamoja na wakulima wa eneo hilo. Kikao hicho kimefanyika katika Bonde la Kibonde Mzungu, Wilaya ya Magharibi ‘B’, Unguja.
\r\n\r\nSaleh amesema lengo kuu la kikao hicho ni kutafuta ufumbuzi wa changamoto zilizowakabili wakulima, ikiwemo kuharibika kwa pampu ya maji hali iliyosababisha kusimama kwa shughuli za kilimo katika bonde hilo.
\r\n\r\nAlisema Wizara kwa kushirikiana na wakulima, Diwani pamoja na Mwakilishi wa Jimbo la Fuoni wamekubaliana kuchangia gharama za ununuzi wa pampu mpya, hatua itakayowezesha kurejea kwa shughuli za kilimo bila vikwazo.
\r\n\r\nAidha, aliwataka wakulima kuhakikisha wanaitunza na kuisimamia vyema pampu hiyo pamoja na miundombinu mingine ya umwagiliaji mara baada ya kununuliwa, ili kulifanya bonde hilo kuwa endelevu na lenye tija kwa uzalishaji wa kilimo.
\r\n\r\n“Nawasihi wakulima mjitahidi kuitunza pampu na miundombinu mingine muhimu ili iweze kudumu na kunufaisha wakulima kwa muda mrefu”, alisema Saleh.
\r\n\r\nHata hivyo, aliwahimiza wakulima kuimarisha ushirikiano na mshikamano hasa pale changamoto zinapojitokeza, jambo litakalosaidia kuzitatua kwa haraka na kwa ufanisi na kuongeza kuwa serikali inatambua mchango mkubwa wa wakulima katika kukuza uchumi wa Taifa na itaendelea kushirikiana na wadau wa sekta ya kilimo kwa kutumia mbinu bora na za kisasa ili kuongeza uzalishaji. Kwa upande wao, Diwani wa wadi ya Fuoni, Farashuu Abdalla na Mwakilishi wa Jimbo hilo, Juma Thabit Kaponda, walisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na wakulima, huku wakipongeza juhudi za Wizara ya Kilimo kufika moja kwa moja katika bonde hilo na kusikiliza changamoto za wakulima. Nao wakulima wa bonde hilo lenye jumla ya hekta 25 na linawahusisha wakulima wapatao 193wameiomba serikali kuendelea kuwaunga mkono kwa kuweka mikakati madhubuti itakayoboresha uzalishaji na kuongeza kipato chao.
\r\nFans
Followers
Followers
Subscribers