Photo

Posted: 2026-04-03

Serikali Yasisitiza Uchinjaji Salama Baada ya Tukio la Nyama Isiyofaa

Description

Jamii imetakiwa kufuata taratibu sahihi za uchinjaji wa wanyama ili kujikinga na maradhi yanayoweza kuhatarisha afya za binaadamu. Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Karantini wa Kisakasaka Hawa Said Kassim Wilaya ya Magharibi ‘B’, kufuatia tukio la kukamatwa kwa nyama ya ng’ombe inayosadikiwa kuibwa, iliyochinjwa kinyume cha taratibu za kitaalamu. Amesema nyama hiyo ilikamatwa katika eneo la Mwanakwerekwe Makaburini kwa ushirikiano kati ya askari wa jamii wa shehia hiyo na askari wa Kituo cha Polisi Mwanakwerekwe, ambapo ilibainika kuchinjwa bila uangalizi wa madaktari wa mifugo. Ameeleza kuwa nyama hiyo haifai kwa matumizi ya binaadamu kutokana na kukiuka taratibu za kiafya wakati wa uchinjaji, huku uchunguzi wa awali ukionesha uwepo wa dalili za maradhi ya kimeta, ambayo ni hatari kwa afya ya watu. Aidha, ameitaka jamii kuzingatia sheria na taratibu za uchinjaji zilizowekwa na Serikali kwa kushirikiana na Idara ya Maendeleo ya Mifugo, ili kulinda afya za wananchi. Nae Mkaguzi Msaidizi wa Polisi wa Kituo cha Mwanakwerekwe pamoja na Mkaguzi wa Shehia ya Mwanakwerekwe, Ali Mohd Kidete, amesema wanaendelea kutoa elimu kwa vijana katika maeneo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuwahamasisha kujikita katika shughuli halali za kujipatia kipato na kuepuka vitendo vya uhalifu kama wizi wa mifugo. Kwa upande wa Sheha ya Shehia ya Mwanakwerekwe, Amani Ayoub Makame, ameeleza kusikitishwa na tukio hilo lililosababisha hasara kubwa, baada ya nyama hiyo kuteketezwa kutokana na kutofaa kwa matumizi ya binaadamu. Amesema hatua hiyo ilichukuliwa katika maeneo maalum yaliyotengwa kwa ajili ya kuteketeza bidhaa zisizokidhi viwango vya matumizi. Sambamba na hilo, amewataka wazazi na walezi kufuatilia mwenendo wa watoto wao ili kuwakinga dhidi ya vitendo viovu vinavyoweza kusababisha hasara katika jamii. Pia amewatahadharisha wananchi kuepuka kununua nyama katika maeneo yasiyo rasmi, kwani hali hiyo huchochea ongezeko la wizi wa mifugo.

\r\n