Photo

Posted: 2026-01-08

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Haroun Ali Suleiman Afunguwa Maabara ya Afya ya Wanyama (ZALIRI)

Description

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Haroun Ali Suleiman, amezindua rasmi Maabara ya Utafiti wa Afya ya Wanyama iliyopo Dole Kizimbani, Wilaya ya Magharibi “A”, kwa kukata utepe, ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za maadhimisho ya miaka 62 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. Amesema Uzinduzi wa maabara hiyo utaimarisha utafiti wa magonjwa ya wanyama, kuongeza usalama wa afya ya mifugo pamoja na kuchangia maendeleo ya sekta ya kilimo na mifugo nchini. Tunafanya jambo zuri la kufungua Maabara hii ni sehemu inayohitajika kuangaliwa kwa umakini kuazia wataalam,wafanyakazi hadi vifaa vya maabara ili viwe endelevu alisema Mhe. Haroun, Amesema ameelezwa kuwa Gharama za Mradi huo ni jumla ya shilingi za kitanzania Bilioni moja na milioni mia mbili (1,200,000,000) ambapo shilingi za kitanzania milioni(450) kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na (750 )kutoka kwa Mfadhili ambaye ni friedrich ya Ujerumani. Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Mhe. Dkt. Salum Soud Hamed, alisema kuwa uwepo wa maabara hiyo utaongeza uwezo wa kitaalamu katika kugundua, kudhibiti na kuzuia magonjwa ya wanyama, hatua itakayosaidia kulinda Mifugo na afya ya binadamu kwa ujumla wake kwa kufuga wanyama na kula nyama zilizotafitiwa na Maabara zetu kwa ubora na ili tuwe na uhakika wa chakula kilicho salama. Aliongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuwekeza katika miundombinu ya utafiti na sayansi ili kuhakikisha sekta ya mifugo inachangia kikamilifu uchumi wa Taifa. Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo na Mifugo Zanzibar, Dkt. Abdallah Ibrahim Ali, alieleza kuwa taasisi hiyo imepiga hatua kubwa katika tafiti za kisayansi, ikiwemo kuongezeka kwa uwezo wa wataalamu, uboreshaji wa mazingira ya utafiti pamoja na matumizi ya matokeo ya tafiti katika kuongeza uzalishaji wa mifugo. Dkt. Abdallah pia alibainisha kuwa taasisi hiyo ina ushirikiano wa karibu na Taasisi ya utafiti ya Ujerumani Friedrich-Loeffler-Institut (FLI) ushirikiano unaolenga kubadilishana uzoefu, kuimarisha tafiti za afya ya wanyama na kukuza taaluma za wataalamu wa ndani. Alimtaja Prof. Saccha Knauf kuwa miongoni mwa wataalamu wanaoshirikiana na taasisi hiyo katika nyanja za utafiti wa kisasa wa afya ya wanyama ikiwa ni wafadhili wa jengo la utafiti wa wanyama vifaa vya kisasa vya utafiti pamoja na kutoa mafunzo kwa wataalamu wa tafiti wa Zaliri. Uzinduzi wa Maabara ya Utafiti wa Afya ya Wanyama Dole Kizimbani unatarajiwa kuwa chachu ya maendeleo ya tafiti za kilimo na mifugo sambamba na kuimarisha juhudi za Serikali katika kulinda afya ya wanyama.

\r\n