Photo

Posted: 2025-12-22

Waziri wa Kilimo na Naibu Waziri Waongoza Zoezi la Usafi wa Mazingira Kaskazini B katika Maadhimisho ya Miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar

Description

Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, akiongozana na Naibu Waziri, wameshiriki katika zoezi la usafi wa mazingira lililofanyika Wilaya ya Kaskazini B, Unguja. Ushiriki huo ni sehemu ya shamrashamra za kuadhimisha miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
\r\nZoezi hilo, lililofanyika katika maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba, lililenga kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika kutunza mazingira safi na salama, sambamba na kuenzi mafanikio ya Mapinduzi ya Zanzibar. Akizungumza katika zoezi hilo la usafi wa mazingira, Waziri wa Kilimo, Mhe. Suleiman Masoud Makame, amesema kuwa katika kipindi hiki kinachotarajiwa kuwa na mvua za masika, ni muhimu kuzingatia suala la usafi. Alieleza kuwa mara nyingi mvua zinapoanza kunakuwa na changamoto za maradhi yanayosababishwa na uchafu katika baadhi ya maeneo, hivyo akasisitiza umuhimu wa kuendeleza usafi wa mazingira kama zoezi endelevu. Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Dkt Salum Soud Hamed, amesisitiza masheha kuendelea kuhakikisha wanawashirikisha wananchi katika utoaji wa elimu ya usafi wa mazingira ili kudumisha dhana nzima ya usafi katika jamii.
\r\nNaye Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini B, Unguja, Mhe. Juma Sururu Juma, amewashukuru wananchi pamoja na viongozi wa wizara kwa kushiriki katika zoezi hilo. Aidha, aliwaomba wananchi kuyaenzi Mapinduzi ya Zanzibar na kuendelea kushiriki katika shughuli mbalimbali kwa amani na utulivu ili kuyadumisha Mapinduzi hayo kwa vitendo.

\r\n