
Kazi za Utafiti wa Kilimo hapa Zanzibar zilianzishwa mnamo mwaka 1910 ambapo mkazo uliwekwa katika kuendeleza utafiti wa mazao ya biashara na mifugo. Kazi chache za utafiti kwa wakati huo zilikuwa zikiendeshwa katika kituo cha kilimo Dunga na vituo vyengine vya Idara ya Kilimo ambayo kwa wakati huo ilikuwa ikiitwa Idara ya Zaraa. Mnamo mwaka 1933 Kituo cha Utafiti wa Kilimo Kizimbani kilianzishwa kwa lengo la kushughulikia tatizo la maradhi ya mikarafuu. Sambamba na kituo cha Kizimbani, pia vilianzishwa vituo vyengine vidogo vidogo (Matangatuani, Makunduchi na Wesha)
Tangu wakati huo hadi sasa eneo la Kizimbani lenye hekta 201 ndio kituo kikuu na makao makuu ya shughuli za utafiti wa kilimo hapa Zanzibar. Maeneo mengine ya utafiti ni Miwani, Selem, Mwera, Kidichi, Bambi na Makunduchi. Kwa upande wa Pemba makao makuu ni Matangatuani na vituo vyengine ni Wesha, Tumbe, Weni na Fundo. Katika miaka ya 1960, utafiti ulianzishwa katika kutafuta mazao mbadala (Hiliki na vanilla) ya kushirikiana na zao la karafuu katika kuimarisha uchumi wa Zanzibar. Baada ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar mwaka 1964 kazi za utafiti wa kilimo ziliimarishwa kwa kutilia mkazo utafiti wa mazao ya chakula kupitia miradi mbali mbali ya maendeleo. Katika miaka ya 1980 shughuli za utafiti wa kilimo ziliwekwa chini ya Kamisheni ya Utafiti na Elimu kwa Wakulima (KUEW). Katika kuongeza msukumo na ufanisi wa kazi za utafiti mnamo mwaka 1991 kulianzishwa Mpango Mkuu wa Utafiti wa Kilimo (ZanzibarAgricultural Research Master Plan) uliotilia maanani matumizi ya mbegu bora, miche ya mazao muhimu, matumizi ya madawa na mbolea, huduma katika mazao baada ya mavuno, uimarishaji wa huduma za mifugo na matumizi ya malisho bora
Katika juhudi za kuimarisha kazi za utafiti wa kilimo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mnamo mwaka 2011 ilianzisha Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (Zanzibar Agricultural Research Institute – ZARI). Aidha, katika juhudi za kuimarisha kazi za utafiti wa kilimo. Serikali ilianzisha Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TUK) mnamo mwaka 2011 kwa kuteuliwa Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, ambapo mwaka 2012 Sheria ya kuanzishwa Taasisi hiyo (Sheria namba 8 ya mwaka 2012) ilitungwa na kuanza kutumika. Taasisi hii ilipewa jukumu la kuendesha kazi zote za utafiti wa sekta ya kilimo (kilimo, mifugo, maliasili na uvuvi). Hata hivyo, mnamo mwaka 2017 sekta ndogo ya mifugo ilienguliwa kwa kuundwa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo(Zanzibar Livestock Reseach Institute-ZALIRI), na baadae sekta ndogo ya uvuvi pia ilienguliwa kwa kuanzishwa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi(Zanzibar Fisheries Reseach Institute-ZAFIRI) mnamo mwaka 2019. Kutokana na mabadiliko hayo, Serikali iliamua kufuta Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Nam. 8 ya mwaka 2012 na kutungwa mpya kwa Sheria namba 8 ya mwaka 2020, ambapo chini ya Sheria hiyo Taasisi ya Utafiti wa Kilimo sasa imepewa jukumu la kuendesha kazi zake katika sekta ndogo za Kilimo na Maliasili tu