SERA YA KILIMO KUSAIDIA KUSIMAMIA UZALISHAJI WA MAZAOPosted: 2024-03-24
Katibu Mkuu kiongozi wa Serekali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhandisi Zeyna Ahmed Said amesema kuwepo kwa Sera ya kilimo kutasaidia kusimamia uzalishaji wa mazao na kuleta mabadiliko ya Sekta ya kilimo. AKIZUNGUMZA katika ukumbi wa ZURA Maisara wakati akifungua kikao cha kupitia Sera ya Kilimo na kupokea maoni kwa Makatibu wakuu na Manaibu katibu wa Mawizara ya Serekali ya Mapinduzi Zanzibar.
Amesema kilimo kina umuhimu Mkubwa katika kuchangia pato la nchi ambapo Zanzibar inaonekana kuwa na eneo dogo la uzalishaji wa mazao ya kilimo hivyo Mipango na mikakati ya kusaidia kilimo inahitajika ili kuweza kuwa na mabadiliko ya sekta kilimo nchini. Aidha amewataka wadau na watunga sera kutoa maoni yao kikamilifu ili kuweza kuwa na sera mpya ya kilimo itakayo kwenda sambamba na mabadiliko na mahitaji ya wananchi,wakulima na wafanyabiasha na kuwa na muelekeo wa kuzalisha mazao kwa malengo na kuachana na ukulima wa kimazowea
Akiwasilisha mada ya mabadiliko ya sera ya kilimo Afisa Mipango Ali Usi Basha amesema kilimo kinamchango mkubwa katika kuhakikisha Usalama na uhakika wa chakula ikiwa bado uzalishaji wetu ni mdogo.hivyo mpango huu wa sera ya kilimo unalenga kuelekea katika uwekezaji ili kupunguza changamato za uhaba wa ardhi,tafiti,wataalamu,maji na pembejeo. Amesema lengo la kuijadili Sera hiyo ni kutokana na hali mabadiliko katika sekta ya kilimo yaliyo tokana na ongezeko la watu, ukuwaji wa teknologia, uvamizi wa maeneo ya kilimo na mabadiliko ya hali ya hewa
Akitoa maoni yake katika kikao hicho Katibu Mkuu Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar Dkt Aboud Suleman Jumbe amesema rasimu ya kilimo ilenge katika mazao ya vipaumbele kwakuwa tunakabiliwa na changamoto za kiuzalishaji hivyo lazima tuoneshe mabadiliko katika sera ili tuweze kuimarisha uzalishaji na kuunganisha mifumo ya katika kuweka mnyororo wa thamani wa mazao na kuweza kuendeleza masoko na utalii kupitia kilimo.