![Photo](../portal/storage/65fc238e62faa9.69294185.jpg)
WAZIRI WA KILIMO SHAMATA SHAAME KHAMIS ASEMA USIMAMIZI WA RASILIMALI ZA MISITU LIBAKI KWA WANANCHI.Posted: 2024-03-21
Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji Maliasili na Mifugo Shamata Shaame Khamis amesema jukumu kubwa la usimamizi wa Rasilimali za Misitu linabaki kwa Wanachi kwani wao ndio watumiaji wakubwa wa rasilimali hizo.
Shamata aliyasema hayo huko katika Maadhimisho ya siku ya Misitu duniani yaliyofanyika Jozani Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.
Alisema jambo hilo litakuwa la busara ikiwa Wananchi wenyewe wataendelea kuilinda, kuitunza na kuihifadhi Misitu kwa vile kukosekana kwake wao ndio waathirika wa hilo.
"Ningependa kutoa agizo kwamba lazima miti tuliyoipanda leo itunzwe vizuri ili Misitu iweze kuimarika na kutoa huduma zinazostahiki, pia tunatakiwa tuchukuwe juhudi kubwa tena za makusudi kupanda miti kwa wingi," alisema Shamata.
Aidha alifahamisha ikiwa watu wanachukua juhudi za kupanda miti katika maeneo ya wazi ikiwemo mashuleni, hoteli, barabarani na sehemu za vikosi lazima lengo ni kurejesha Zanzibar ya kijani lifikiwe.
Shamata alikemea kuhusu uharibifu unaofanywa na baadhi ya wanajamii wanaokata misitu ovyo kwa kutumia misumeno ya moto na kusafirisha mazao bila kufuata taratibu zilizopo
Akiwa katika sehemu ya upandaji wa miti huko katika kijiji cha charawe Waziri huyo alisema uharibifu wa mazingira umepelekea kuongezeka kwa joto na kupelekea ongezeko kubwa la mabadiliko ya tabianchi.
Alifahamisha kuwa jukumu la utunzaji wa mazingira na upandaji wa miti ni jukumu la kila mmoja sio la watu fulani hivyo wakati umefika kwa vijana na wanafunzi kuwa tayari katika upandaji wa miti na utunzaji wa mazingira.
Alitoa wito kwa jamii waishio karibu na misitu kwa yeyote atakaye kamatwa ametenda makosa atawajibishwa kisheria bila ya kuonewa huruma.
Naye, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Ali Khamis Juma alisema jumla ya Sh512,815,155 milioni na Dola za kimarekani 25,598,37 zimetolewa katika kilele hicho kwa wadau wa hifadhi ya taifa ya Jozani, ikiwa ni mapato yanayotokana na utalii katika Msitu wa hifadhi hiyo kwa kipindi cha miezi sita kuanzia July hadi disemba 2023.
Alisema, Wizara yake imekua ikichukua jitihada za dhati ili kuhakikisha mapato hayo yanaongezeka ili mgao huo uwe mkubwa na kuzidi kutoa tija kwa Serikali na wadau husika.
Akisoma risala, Mwenyekiti wa Kamati ya Uhifadhi Shehia ya Pete, Wahida Mohd Ali alisema mikataba inayosimamiwa na wananchi inakabiliwa na changamoto kutokana na kuongezeka na kwa idadi watu na mahitaji yao.
"Sisi wananchi wa Pete tuna ombi kuhusu Mikataba ya CoFMA ambayo imelenga kuwapa fursa wanajamii kusimamia Misitu yao. Mikataba hii inakabiliwa na changamoto kubwa kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu na mahitaji yao,"alisema.
Mwisho.