WANAFUNZI WAPATA ELIMU YA MISITU KUELEKEA MAADHIMISHO YA SIKU YA MISITU DUNIANI 2024Posted: 2024-03-19
Msaidizi Mkuu wa Hifadhi ya Kimaumbile ya Masingini Amour Khamis Juma amesema ipo haja kwa Jamii na Wanafunzi kuwashirikisha katika utoaji wa Elimu ili kujua umuhimu wa Misitu na kutambua rasilimali zilizopo ikiwemo wanyama, ndege na miti adimu sambamba na kuhifadhi mazingira kwa ujumla.
Hayo ameeleza huko katika hifadhi ya kimaumbile ya masingini wakati alipokua akitoa elimu kwa wanafunzi wa skuli ya Mtoni Kigomeni, skuli ya Bububu ‘A’ na Mtopepo ‘B’ kwa kuelekea maadhimisho ya kilele cha Siku ya Misitu Duniani inayoadhimishwa Machi 21 ya kila mwaka.
Amour alieleza kuwa siku hiyo huadhimishwa kwa lengo la kuelimisha jamii wakiwemo wanafunzi juu ya umuhimu wa kutunza mazingira kwa kupanda miti, kutunza misitu kuwapa hamasa wanajamii pamoja na kutunza Mazingira kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Aidha alisema maadhimisho hayo yalianza kuasisiwa na Shirika la Chakula Duniani (FAO) mwaka 2016 ambapo ikiwa na dhamira ya kuwaeleza Wanajamii juu ya Umuhimu wa Utunzaji wa Miti Duniani.
"Katika maadhimisho haya wafanyakazi wa Idara ya Misitu tunaadhimisha siku hiyo kwa kupanda miti katika maeneo tofaut ya Hifadhi lakini kwa mwaka huu tutaadhimisha kwa kufanya mambo tofauti ikiwemo la kuelimsha wanafunzi katika misitu yetu na hifadhi ya taifa ya Jozani", alisema Amour .
Hata hivyo alifahamisha kuwa kilele cha maadhimisho hayo kitajumuishashughuli za upandaji miti ya mikoko katika hifadhi ya taifa Jozani katika shehia ya Charawe na kuzinduliwa mradi wa kitalii wa mnara wa shehia ya Pete na Ugawaji wa hundi kwa wadau wa hifadhi hiyo.
Kwa upande wake mwalimu wa skuli ya msingi Bububu ‘A’, Khatib Hamad Khatib, kwa niaba ya walimu wenziwe wamesema wamehamasika na upewaji wa elimu kwa wataalamu wa Misitu kwani wameweza kujua umuhimu wa kuhifadhi Misitu na Faida zake
Nao wanafunzi wamesema wamefurahishwa kupata taaluma nzuri ya Kujifunza Kuhusiana na uwepo wa Hifadhi ya Misitu na kuwaomba wale wote ambao wanaokata miti pindi wanapoikata wajitahidi kuirudisha miti hiyo na kua katika hali nzuri kwani kufanya hivyo kutapelekea athari za mmong’onyoko wa ardhi katika hifadhi za misitu.
Shamra shamra za kuelekea Siku ya Misitu duniani hufanyika kila mwaka ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘Misitu ni Ubunifu, ni Suluhisho jipya kwa Dunia Bora’.