
WAZIRI SHAMATA ATEMBELEA UJENZI WA MIUNDOMBINU YA UMWAGILIAJI MAJI CHEJU Posted: 2024-03-16
Waziri wa Kilimo Umwagiliaji Maliasili na Mifugo Mheshimiwa Shamata Shaame Khamis amemtaka Mkandarasi anaehusika na Ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji maji ikiwemo Uchimbaji na utengenezaji wa Visima katika bonde la Cheju B kuhakikisha Ujenzi unamaliza kwa wakati ili Wakulima waweze kurudi katika mabonde yao na kuendelea na kilimo.
Hayo ameyasema huko bonde la Cheju B Wilaya ya Kati Unguja ikiwa ni Ziara ya kuangalia Ujenzi unaoendelea kujengwa ktk bonde hilo
Amesema lengo la Ziara hiyo ni Kuona Utekelezaji wa Mradi huo unavyopiga hatua katika ujenzi wa bonde hilo ikiwa ni Program ya Miundombinu ya Umwagiliaji kwa awamu ya pili ya mkopo kutoka Exim Benki ya Korea ya dola za Kimarekani 18.1 pindi ukikamilika kama ulivyopangwa utaweza kuwawezesha Wakulima waweze kulima kwa wakati
Aidha Shamata amemsisitiza Mkandarasi huyo kuhakikisha wanamaliza Ujenzi huo ili Wakulima wasisitishe shughuli za kilimo kwa mda mrefu kwa vile dhana ya Serikali ni kuona Upatikanaji wa uhakika wa Chakula unaimarika siku hadi siku.
Kwa Upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Ali khamis Juma amesema pamoja na kuangalia shughuli za Ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji maji ikiwemo Visima lakini pia ipo haja kwa Wafugaji wenye tabia ya kufunga Wanyama wao katika Mabonde ya Mpunga Waache tabia ya kuingiza Mifugo yao katika mashamba ya kilimo.