SERIKALI YA MAPINDUZI ZANZIBAR ITASHIRIKIANA NA WADAU WA KIMAENDELEO KATIKA TAFITIPosted: 2024-03-14
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Wadau wa kimaendeleo katika tafiti kwa nia ya kuongeza uzalishaji wa mazao ya mboga mboga na kuwajengea Uwezo Wakulima ili Kuongeza kasi ya Uchumi Nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo ZARI Dkt. Mohamed Dhamir Kombo ameyasema hayo huko katika Ukumbi wa Taasisi hiyo Kizimbani wakati alipofungua Mafunzo kwa Wakulima ya Uzalishaji wa mbegu bora za mboga mboga.
Alisema Serikali imepiga hatua kubwa katika kuimarisha Miundombinu ya kisasa ili Kuongeza Uzalishaji na kuwa na Ongezeko la Chakula Nchini.
"Tumeambiwa itakapofika mwaka 2030 Dunia itakua na Watu zaid ya Billioni 9 hivyo Mahitaji ya chakula yataongezeka zaidi kwahiyo niwaombe Wakulima mlioshiriki katika Mafunzo mufikishe Elimu mliyoipata kwa wenzenu ili muweze kutumia mbinu bora na kuhakikisha tunaongeza Uzalishaji wa kutosha ili kukabiliana na Ongezeko la watu" Alisema Mkurugenzi huyo.
Alifahamisha kuwa Serikali ya awamu ya nane inayoongozwa na Dk Hussein Ali Mwinyi pamoja na Wasaidizi wake wana nia njema na wananchi wao katika kuhakikisha wanawezeshwa kwa miundombinu ya uzalishaji na taaluma ili waongeze Uzalishaji wenye tija na kutatua Changamoto zinazowakabili Wakulima ili kuweza kujitosheleza kwa Chakula.
Nae Afisa Mradi wa World Vegetable Center Nickson Mlowe aliongeza kwa kusema Mafunzo hayo yamelenga kuwa na mashamba darasa 12 kwa Upande wa Unguja na kwa Upande wa Pemba kuwe na mashamba darasa 8 hivyo Wakulima watapata kujifunza namna ya kuzalisha mbegu bora kwa maana ya kuvuna na kusarifu.
Kwa Upande wake Mkuu wa Kitengo cha Maendeleo ya Utafiti na Uratibu ZARI bi Khadija Ali Juma alieleza kuwa Wakulima wa Zanzibar wanatumia mifumo rasmi na isiyo rasmi katika Upatikanaji wa mbegu ambao hugawana wenyewe kwa wenyewe mbegu ambazo hazikaguliwi hivyo kwa Sasa Serikali iko katika Mchakato wa kutengeneza Sheria ya Mbegu ambayo itaweza kusaidia kurasimisha Uzalishaji na Usambazaji wa Mbegu kwa Wakulima.
Nao Wakulima walisema kwa sasa wanakabiliwa na Changamoto ya Maji katika Mashamba yao, Ukosefu wa Uhifadhi wa mbegu hivyo wameiomba Wizara ya kilimo kupitia Taasisi hiyo kuwatatulia Changamoto hizo zilizopo kwani matarajio yao baada ya Mafunzo hayo ni kupata Uzalishaji wa mazao mengi na yenye kuleta tija.
Mafunzo hayo ya siku mbili yameandaliwa na World Vegetable Center kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo na kuwashirikisha Wakulima Kutoka katika Maeneo mbali mbali ya Unguja chini ya Ufadhili wa USDA.