
MAJAA MITAANI YAZIDISHA ONGEZEKO LA MBWAPosted: 2024-03-14
KUWEPO kwa majaa mengi ya taka kumetajwa kuwa ni miongoni mwa mambo yanayochangia kuwepo kwa mbwa wengi mitaani hali inayosababisha baadhi ya mbwa kukosa tiba ya chanjo kwa wakati kutokana na kutokua na wamiliki.
Akitoa taarifa ya chanjo ya kichaa cha mbwa iliyotolewa na Idara ya Maendeleo ya Mifugo, Daktari Mkuu wa wanyama katika idara hiyo, Dk. Ali Zahran Mohamed, alisema kwa mwaka huu idara yake imeendesha zoezi la uchanjaji na mbwa wapatao 3,616 walipatiwa huduma hiyo katika wilaya zote kisiwa cha Unguja.
Dk. Ali alisema idara hiyo ilijipanga vyema kufikia malengo yake kwa asilimia mia moja lakini kutokana na Uwepo wa mbwa wazururaji kuwakosa wameweza kuchanja na kufikia asilimia 90.6.
Alieleza kuwa katika utoaji wa chanjo hizo bado wanaendelea kutoa chanjo bure kwa kila mwaka ili kuepusha athari za kichaa cha mbwa kisiweze kujitokeza na kuathiri wengine sambamba na kuweza kumuathiri binadamu
Alisema kuwa ipo haja kwa wananchi wanaofuga mbwa kupeleka wanyama wao wakapate chanjo kwa vile Idara inachukua juhudi ya kuhakikisha mbwa wote wanapewa chanjo kwa kiasi kikubwa ili kupunguza madhara.
"Niwaombe wananchi hasa wale wanaofuga mbwa endapo wataskia tangazo la utoaji chanjo wasipuuze badala yake wawafikishe wanyama wao katika vituo husika ili kuwakinga dhidi ya maradhi mbali mbali ambayo mengine yana madhara kwa binadamu ", alisema Dk. Ali.
Aliongeza kuwa idara imejipanga kuanzisha utoaji wa elimu kwa jamii kupitia katika vyombo vya habari Idara kwa kuandaa vipindi vya Radio na Televisheni ili jamii ipate uelewa zaidi kwani itarahisisha kufahamu umuhimu wa chanjo kwa wanyama wote.Naye Mkuu wa Kitengo cha Tiba na Ufuatiliaji wa Mifugo, Asha Ibrahim Khator, alizitaja dalili za mbwa mwenye kichaa ni pamoja na kutokwa mate mara kwa mara, kuogopa maji na mwangaza, kukimbia bila sababu yoyote na hua anabweka sana.
Kwa Upande wa Mfugaji kutoka Kiombamvua wilaya ya Kaskazini ‘B’, Issa Abdallah Salum, aliishukuru Idara ya Maendeleo ya Mifugo kwa mashirikiano waliyompatia katika utoaji wa chanjo kwa wanyama wake na kuiomba Idara hiyo kuwapatia elimu wafugaji wengine wanaopuuza muitikio wa uchanjaji wa mbwa wao
Alieleza kuwa ili kuwanusuru wanyama na maradhi ya kichaa cha mbwa ni muhimu wafugaji wakatimiza wajibu wao kwani chanjo ni kinga inayotolewa na Wizara ya kilimo Umwagiliaji Maliasili na Mifugo kwa kushirikiana na Shirika la Afya linalozuia maradhi ya kichaa cha mbwa Duniani.