
SERIKALI YA MAPINDUZI ZANZIBAR YAWASHAURI WAKULIMA KUJIANDAA NA MSIMU WA MASIKAPosted: 2024-03-14
Kufuatia Utabiri wa Hali ya Mvua kwa kipindi cha Masika 2024, Wizara ya Kilimo Umwagiliaji Maliasili na Mifugo imewashauri Wakulima kuandaa mashamba, kupanda, kupalilia pamoja na kutumia Pembejeo kwa wakati ili kuepuka athari za mvua ya Masika zinazotarajiwa kunyesha katika Visiwa vya Zanzibar.
Hayo ameyasema Mkurugenzi wa Idara ya Mipango Sera na Utafiti, ndugu Makame Kitwana Makame huko katika Ukumbi wa Wizara hiyo Maruhubi wakati alipokua akijadili na Wakurugenzi pamoja na watendaji wakuu kuhusiana na mwelekeo wa mvua hizo, ambazo zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani kwa mwaka huu.
Amesema ili kukabiliana na hali ya mvua, wakulima wanashauriwa kuzingatia mbinu za kukinga mashamba kwa makingamaji ili kuepuka mafuriko na kuepuka kutuwama kwa maji.
Aidha, Mkurugenzi huyo amesisitiza kwa wale ambao wanatarajia kupanda miti ya kudumu kusubiri mvua zichanganye vizuri ili kuepusha miti yao kufa kutokana na ardhi kutoshiba Maji.
Kwa upande wao, Wakurugenzi wa Wizara hiyo wamesema kwamba kila mmoja kwa Idara yake atachukua hatua za kuwaelimisha wakulima na Taasisi nyengine juu ya Angalizo la Athari za Mvua za masika zinazotabiriwa kuanza kunyesha katika wiki ya mwisho ya mwezi Februari hadi mwezi Mei 2024.