
UZINDUZI WA LISHE ZANZIBARPosted: 2022-06-08
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo pamoja na Shirika la Chakula Duniani (FAO) kwa ufadhili wa Nchi za Ulaya (EU), wamezindua kampeni ya Lishe bora Zanzibar ambayo ilifanyiaka katika viwanja vya bustani ya Forodhani Zanzibar saa 10 jioni tarehe 29/05/2022.
Kampeni hiyo ilizinduliwa na Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar Mhe. Shamata Shaame Khamis, alisema muongozo wa chakula utawezesha Serikali kutekeleza mpango wa kuimarisha afya za wananchi wa Zanzibar.
Aidha, Mhe. Waziri alisema muongozo huo una kwenda sambamba na vipaumbele vya Serikali katika kupunguza utapia mlo na kuwa na taifa bora. Amesema utekelezaji wa lishe utaimarisha afya ya jamii na kupunguza maradhi hasa ya kuipunguzia serikali mzigo wa kusafirisha wagonjwa nje ya nchi.
Mhe. Shamata ameeleza ripoti ya lishe nchini imeonesha udumavu umepungua kutoka asilimia 23 ya mwaka 2015 na kufikia asilimia 21 ya mwaka 2018, hivyo amewataka wananchi kutumia vyakula vya lishe ili kuimarisha afya zao.
Nae mwakilishi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa la FAO nchini Tanzania Dkt. Nyambenyi Tipo amesema wakati umefika kwa watanzania kutumia mlo bora na kuwataka wananchi wabadilike kwa kuzalisha na kula chakula cha kuimarisha afya zao.