
UTANGULIZI
Wakala wa Serikali wa Huduma za Matrekta na Zana za Kilimo ni miongoni mwa Taasisi kumi na nne za Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi katika kipindi cha pili cha awamu ya saba inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Ali Mohammed Shein (2015-2020). Wakala wa Serikali wa Huduma za Matrekta na Zana za Kilimo umeanzishwa kwa mujibu wa Sheria Namba 2 ya 2019 na inatekeleza majukumu yake kama yalivyoainishwa kwenye Sheria tuliyoitaja hapo juu.
Wakala wa Serikali wa Huduma za Matrekta na Zana za Kilimo unatekeleza majukumu yake katika Vituo vyake vikubwa viwili; Kwa upande wa Unguja, kituo kipo Mbweni – ambapo hapo ndio Makao Makuu ya WAKALA, na kwa Pemba, Kituo kipo Wawi. Eneo la WAKALA la Mbweni Unguja lina ukubwa wa hekta 2.91 (Ekari 7.25) na lile la Wawi Pemba lina ukubwa wa mita za mraba elfu nne na mia saba (4700m2), sawa na wastani wa ekari 1.25
HISTORIA YA WAKALA
Baada ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar (1964), Rais wa kwanza Marehemu Mzee Abeid Amani Karume alitilia mkazo sana kilimo cha mazao ya chakula na kutoa kipaumbele zaidi katika kilimo cha mpunga. Mnamo mwaka 1966, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilipata msaada wa matrekta 50 kutoka Jamhuri ya Watu wa China pamoja na majembe yake ya kuchimba na kuburuga. Lengo la zana hizi ilikuwa ni kuwapunguzia mzigo wakulima ambao walikuwa wakilima kwa kutumia jembe la mkono. Sambamba na msaada huo, Karakana ya matrekta ilijengwa hapo Mbweni, Zanzibar kwa ajili ya kutoa huduma za kiufundi kwa matrekta na zana zake.
Kutokana na mtazamo wa uendeshaji uchumi wa wakati huo, Karakana hii ilikuwa ipo chini ya Wizara ya Kilimo na ikitoa huduma kwa Wizara hiyo. Kwa kipindi chote hicho, uingizaji wa fedha kwa karakana ulikuwa ni mdogo ukilinganisha na bajeti iliyokuwa ikitengwa pia hakukuwa na malipo yoyote yaliyotolewa kwa matengenezo ya matrekta yaliyokuwa yakifanywa na Karakana. Hali hii ilipelekea karakana kushindwa kujiendesha kutokana na ukosefu wa fedha na uchakavu wa zana za kufanyia kazi.
Mnamo mwaka 1980 Serikali ilianzisha Mradi wa Kuirudishia Uwezo Karakana ya Matrekta (Zanzibar Tractor Repair Wokshop Rehabilitation Project) kwa kuyatengeneza baadhi ya matrekta yaliyoharibika, chini ya uhisani wa Serikali ya Uholanzi, mradi ambao uliendelea hadi mwaka 1991. Mradi ulipendekeza Karakana ibadilishwe muundo wake na kuwa Taasisi inayojitegemea ili kuweza kuendeleza kazi zake za kuyahudumia matrekta na kuzitunza mashine zilizopo baada ya mradi kumalizika. Mara baada ya kumalizika kwa mradi (1991) Serikali ilibadilisha muundo wa Karakana ya Matrekta Mbweni na kuifanya kuwa ni Taasisi inayojitegemea ikiwa na muundo unaofanana na Shirika. Aidha, katika kipindi hichi cha kuwa Taasisi inayojitegemea, Serikali iliteua Meneja Mkuu, uanzishaji wa Bodi ya Karakana na kubadilisha umiliki wa vyombo vya usafiri kutoka kwa Wizara na kuwa vya Shirika. Katika kipindi hiki chote, Shirika lilikuwa linajitegemea wenyewe isipokuwa mishahara ilikuwa inatoka Serikalini kupitia Wizara ya Kilimo. Kutokana na kutokuwepo Sheria, muundo madhubuti, mikakati ya uendeshaji, ukosefu wa fedha na uchakavu wa zana, Karakana ilishindwa kujiendesha na kupelekea mwaka 2011 kurejeshwa na kuwa kitengo chini ya Idara ya Kilimo.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kutekeleza Mikakati yake ya mageuzi ya kiuchumi na kijamii yenye lengo la kupunguza umasikini na kuongeza pato la Taifa kufikia nchi yenye uchumi wa kati, kwa kuandaa mazingira mazuri ya uhakika wa chakula na lishe bora kwa wananchi, ilionekana upo umuhimu wa kuanzisha Wakala wa Serikali wa Huduma za Matrekta na Zana za Kilimo. WAKALA ambao utawezesha wananchi kuondokana na utegemezi wa zana duni za kilimo na kuweza kufanya kilimo kuwa endelevu, cha kibiashara na chenye tija zaidi. Kuimarisha uendeshaji wa Karakana, kuwajenga uwezo wafanyakazi na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi. Kwa mantiki hiyo na kwa kutumia uwezo wa Mhe. Rais wa Zanzibar kwenye Kifungu Namba 53 cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na Kifungu Namba 55 cha Sheria Namba 2 ya 2011 ya Utumishi wa Umma, Wakala wa Serikali wa Huduma za Matrekta na Zana za Kilimo ulianzishwa kwa kutumia Hati ya Kisheria Namba 55 ya 2017 (Legal Notice No. 55 of 2017).
WAKALA iliagizwa na Baraza la Mapinduzi kutayarisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu yake na kuiwasilisha taarifa hio Baraza la Mapinduzi. WAKALA ilitayarisha taarifa husika na kuiwasilisha Baraza la Mapinduzi kama ilivyotakiwa kufanya hivyo. Pamoja na hayo, baada ya Baraza la Mapinduzi kuijadili taarifa husika, kwa pamoja waliwaagiza Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi kuunda Sheria ya kuanzishwa kwa WAKALA badala ya Hati ya Kisheria iliopo.
Katika kutekeleza agizo hilo la Baraza la Mapinduzi, Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi iliwaagiza WAKALA kutayarisha rasimu ya Sheria husika kwa kufuata utaratibu ulioagizwa na Serikali. WAKALA walitayarisha Rasimu ya Sheria na kuiwasilisha Rasimu hio ya mwanzo ya Sheria ya kuanzishwa kwa Wakala wa Serikali wa Huduma za Matrekta na Zana za Kilimo kwa Bodi ya Ushauri ya WAKALA katika kikao chake cha kawaida kilicho fanyika Ofisi za WAKALA zilizopo Mbweni - Zanzibar. Baada ya Bodi kuijadili Rasimu hiyo ya Sheria, Rasimu hio ilipelekwa kwa Kamati ya Uongozi ya Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi kwa kupitiwa na kutolewa muongozo. Baadae Rasimu ya Sheria ilifuata utaratibu kama Serikali inavyoelekeza katika utungaji wa Sheria; Ikiwa ni pamoja na kupitiwa na Kikao cha Makatibu Wakuu, Baraza la Mapinduzi na hatimae Baraza la Wawakilishi kwa kujadiliwa na kupitishwa.
Mswada wa Sheria ya kuanzishwa kwa Wakala wa Serikali wa Huduma za Matrekta na Zana za Kilimo ulipelekwa Baraza la Wawakilishi kwa ajili ya kusomwa na kujadiliwa na hatimae ulipitishwa. Sheria ya WAKALA ilikamilika utungwaji wake na Mhe. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliitia saini rasmi Sheria hio siku ya tarehe 7 Mei, 2019, na kujulikana kuwa SHERIA NAMBA 2 YA 2019 YA KUANZISHWA KWA WAKALA WA SERIKALI WA HUDUMA ZA MATREKTA NA ZANA ZA KILIMO. Kwa mnasaba wa maelezo hayo, kwa sasa Wakala wa Serikali wa Huduma za Matrekta na Zana za Kilimo unatekeleza majukumu yake kulingana na matakwa ya Sheria iliyotajwa hapo juu.
Katika utekelezaji wa majukumu yake, Wakala wa Serikali wa Huduma za Matrekta na Zana za Kilimo unaongozwa na Sheria Namba 2 ya 2019, Dira ya Maendeleo ya Zanzibar (Zanzibar Vision 2020), Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUZA III), Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), Mipango Mikakati ya Kisekta pamoja na Mpango wa Mageuzi wa Sekta ya Kilimo (ATI), Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Kilimo Zanzibar - ZASDP (2019 – 2029), ILANI ya Uchaguzi ya CCM 2015 – 2020, pamoja na Sheria na Sera mbali mbali za Wizara.