
UTANGULIZI
Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Zanzibar (Zanzibar Livestock Research Institute– ZALIRI), ilianzishwa tarehe 12 May, 2017 kwa Hati ya Sheria (Legal Notice) Nam. 45, ya tarehe 12 Mei, 2017.
MAKAOMAKUU YA TAASISI
Makao Makuu ya Taasisi ya mifugo ipo katika kijiji cha Dole umbali wa kilometa 15 kutoka Mjini, wilaya ya magharibi “A” mkoa wa Mjini Magharibi. Ofisi ndogo ipo chamanangwe Pemba kijiji cha Kiuyu Wilaya ya Wete.
MANTIKI YA KUANZISHWA TAASISI
Sekta ya Mifugo nchini imechangia asilimia 2.8 ya pato la Taifa kwa mwaka 2018. Sekta hii inayo uwezo mkubwa zaidi wa kuchangia katika uchumi wa nchi yetu, kupunguza umaskini na kuimarisha uhakika wa chakula na lishe bora, isipokuwa inakabiliwa na changamoto nyingi za maradhi, malisho, chakula duni cha mifugo, masoko n.k. Kutokana na changamoto hizi, Serikali imeona ipo haja ya kufanya marekebisho ya Mpango Mkuu wa Utafiti wa Kilimo kwa kuimarisha tafiti za kilimo na mifugo. Kutokana na hilo, imeanzishwa Taasisi hii ili kuzipatia ufumbuzi changamoto za sekta ya mifugo kwa kusimamia utafiti na kubuni teknolojia za kisasa zitazoleta maendeleo ya sekta ya mifugo na kukuza mchango wake katika uchumi wa nchi yetu.
Uanzishwaji wa Taasisi umeelekezwa katika mipango ya maendeleo ya Zanzibar. Zanzibar Research Agenda 2015-2020, MKUZA III, Vision 2020 na Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2015-2020, ambazo zimeelekeza mikakati muhimu ya kuendeleza utafiti katika Sekta ya mifugo. Aidha, tangu ilipoanzishwa mwaka 2017, Taasisi imetekeleza majukumu mbalimbali na kupiga hatua katika kufanya tafiti zinazotatua changamoto za mifugo sambamba na kuimarisha miundombinu ya Taasisi.
- Dira ya Taasisi – Kuwa na taasisi yenye ubora wa kimataifa katika utafiti wa mifugo.
- Dhamira ya Taasisi - Kuzalisha na kukuza teknolojia, maarifa, na ubunifu endelevu wa sekta ya mifugo kwa ustawi wa Zanzibar.
- Lengo la Taasisi - Kuchangia katika kukuza uchumi kwa kuendeleza sekta ya mifugo nchini kwa njia ya utafiti na kubuni teknolojia za kisasa na kuzipeleka kwa wadau.