
WIZARA YA KILIMO UMWAGILIAJI MALIASILI NA MIFUGO KUPITIA IDARA YA MAENDELEO YA MIFUGO, IMEELEZA KUWA ITAENDELEA KUTOA CHANJO YA MARADHI YA KICHAA CHA MBWA ILI KUIAKINGA JAMII NA MADHARA YA MARADHI HAYO.Posted: 2025-01-20
WIZARA ya Kilimo Umwagiliaji Maliasili na Mifugo kupitia Idara ya Maendeleo ya Mifugo, imeeleza kuwa itaendelea kutoa chanjo ya maradhi ya kichaa cha mbwa ili kuiakinga jamii na madhara ya maradhi hayo.
Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Mifugo, Asha Zahran Mohammed aliyasema hayo huko Ndijani Mseweni wakati wa uzinduzi wa zoezi la utoaji chanjo ya ugonjwa wa kichaa cha mbwa kwa ajili ya kuzuia maambukizi ya maradhi yanayoweza kuwakabili mbwa na wanyama wengine wanaofugwa.
“Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina lengo la kutunza jamii yao ili kunusuru maradhi hayo yasiwapate binadamu na ndio maana zoezi la chanjo hiyo hutolewa bure bila ya uwepo wa malipo yeyote kwa wanyama hao”, alieleza Mkurugenzi huyo.
Asha aliongeza kuwa Wizara kupitia Idara yake imejipanga vyema ili kutokomeza maradhi hayo na kuhakikisha mbwa wote wanachanjwa kila mwaka kupitia zoezi kama hilo na kwa wafugaji watakaokosa chanjo hiyo wanatakiwa kufika katika kituo cha mifugo ili wanyama wao wapatiwe chanjo hiyo.
Naye Daktari wa Mifugo Mkuu wa Mifugo Ali Mohammed Zahran, alisema ugojwa huo hauna dawa bali unaweza kuzuiliwa kwa kutumia chanjo kwani maradhi hayo yanapompata binadamu huwa hayana tiba mahsusi badala yake hueza kusabisha kifo.
Mapema Sheha wa Ndijani Mseweni, Masoud Said Abdallah, alisema amepokea zoezi hilo na kuwashukuru madaftar wa mifugo kufika katika shehia yao kwani Wafugaji wengi waliopo katika eneo hilo wanachanja mbwa wao kila mwaka ili mbwa wao waweze kubaki salama.
Nao wafugaji walioshiriki zoezi hilo wameishukuru serikali kwa kuwaletea chanjo hiyo na kuwataka wafugaji wenzao kuwashughulikia mbwa wao na kuwafiksha katika maeneo yaliyopangwa kupatiwa chanjo ili kuwanusuru na maradhi yanayohatarisha usalama wao na jamii kwa ujumla.
Zoezi hilo linatarajiwa kufanyika katika wilaya ya Kati Unguja, Kaskazini ‘A’, wilaya ya Kaskazini ‘B’, wilaya ya Kusini, wilaya ya Magharibi ‘A’, Wilaya ya Magharibi ‘B’ na wilaya ya Mjini kwa Unguja kabla ya zoezi kufanyika na wilaya zote za Pemba.