
KATIBU MKUU WIZARA YA KILIMO, UMWANGILIAJI, MALIASILI NA MIFUGO ALI KHAMIS JUMA AMESEMA MPANGO WA MAGEUZI YA KILIMO UMELENGA KUWAFIKIA WAKULIMA NA WAFUGAJI KATIKA WILAYA ILI KUWASONGEZEA HUDUMA NA UTAALAMU KATIKA KULETA MABADILIKO YA SEKTA YA KILIMO NCHINI.Posted: 2024-12-05
Katibu Mkuu wizara ya kilimo, Umwangiliaji, Maliasili na Mifugo Ali khamis juma amesema mpango wa Mageuzi ya kilimo umelenga kuwafikia wakulima na wafugaji katika Wilaya ili kuwasongezea huduma na utaalamu katika kuleta mabadiliko ya sekta ya Kilimo nchini.
Hayo aliyasema leo wakati akifungua Mkutano wa wadau wa kujadili Mageuzi ya Kilimo kwa wataalamu, Jumuiya za kilimo Tasisi za Serikali na binafsi uliyofanyika katika ukumbi wa Shekh Iddrisa Abdul-Wakil Kikwajuni Zanzibar.
Alisema Mageuzi ya kilimo ni Mpango wa miaka10 utakaoaza kutekelezwa mwazoni mwa mwaka 2025 unalenga kuboresha maisha ya wakulima kwa kuwapatia mafunzo, ujuzi, na vifaa vya kisasa pamoja na kuwepo kwa Vituo maalum vya kilimo katika kila wilaya ili kutoa muongozo kwa wakulima na wafugaji.
"Kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wetu. Sasa ni wakati wa kuachana na kilimo cha mazoea na kuelekea katika kilimo cha biashara, hasa kwenye mazao ya muda mfupi yenye faida kwa wakulima.
Pia aliwataka wadau wa kilimo kushiriki kikamilifu kwa kutoa maoni na ushauri ili mpango huo uweze kutekelezwa kwa mafanikio. Na kusisitiza umuhimu wa kuzitumia fursa za masoko ya kitalii na biashara ambazo bado hazijafikiwa na wakulima wengi wa Zanzibar.
Akitoa mada ya Mageuzi katika Mkutano huo Afisa Mipango kutoka Wizara ya kilimo Ali Usi Basha alisema mageuzi haya yanatarajiwa kuleta mapinduzi ya kilimo Zanzibar, huku yakichochea maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi na kuongeza tija katika sekta ya kilimo.
Amesema Serikali imeweka miundombinu ya barabara na masoko ambapo imerahisisha kuyafikia mashamba kwa urahisi,hata hiyo bado hatujaweza kufikia frusa za mageuzi na kulima kwa lengo la biashara.
Nao washiriki wa Mkutano huo wameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Kilimo kwa kuandaa mpango wa Mageuzi wenye matumaini ya kukibadilisha kilimo hasa kwa vijana ambao itatoa frusa za elimu ya kilimo,pembejeo na mikopo ambazo zitasongezwa katika Mawilaya na kutanua wigo katika kuleta mabadiliko na kuwa na kilimo chenye manufaa.