
WAZIRI WA KILIMO, UMWAGILIAJI, MALIASILI NA MIFUGO, MHE. SHAMATA SHAAME KHAMIS, AMEWASISITIZA WAKANDARASI NA WASIMAMIZI WANAOTEKELEZA MRADI WA UJENZI WA MIUNDOMBINU YA UMWAGILIAJI KUMALIZA KAZI HIYO KWA WAKATI .Posted: 2024-11-14
Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Shamata Shaame Khamis, amewasisitiza Wakandarasi na Wasimamizi wanaotekeleza mradi wa ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji kumaliza kazi hiyo kwa wakati uliopangwa na kuhakikisha miundombinu hiyo inakua imara na yenye tija iliyokusudiwa.
Shamata alitoa maelekezo hayo huko Cheju, wilaya ya Kati Unguja baada ya kukagua ujenzi wa miundombinu hiyo katika bonde la Cheju ‘B’ kwa lengo la kukagua hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mradi huo.
Amesema lengo la kujengwa kwa miundombinu hiyo ni kuwasaidia wakulima kuongeza uzalishaji katika kilimo cha mpunga na mazao mengine sambamba na kuhakikisha usalama wa chakula nchini.
Aidha amewasihi Wakandarasi hao pamoja na Wasimamizi wa mradi huo kuhakikisha kuwa Mhe. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ametoa fedha za kugharamia mradi huo ili kuiendeleza sekta ya kilimo na kusisitiza kuwa Wizara itaendelea kusimamia utekelezaji wa mradi huo ili ulete tija na kuwaondolea shida wananchi.
Kwa upande wake Mshauri elekezi wa ujenzi huo kutoka kampuni ya KRC, Jang Jengryeol, amesema kwa sasa mradi huo umefikia asilimia 99 za utekelezaji na kazi zilizobaki ni kuweka bomba za maji pamoja na uungaji wa umeme mkubwa katika visima.
Kwa Upande wake Mwenyekiti wa bonde hilo, Khatib Kassim Khatib na Katibu wa bonde hilo, Kassim Mdunga wameahidi kuendelea kutoa ushirikiano katika ujenzi unaoendelea kwa kusimamia ipasavyo na kuwashajihisha wakulima wenzao kuweza kutunza Miundombinu katika eneo hilo.
Jumla ya Dola za Marekani 10,462,445 zinatarajiwa kutumika katika ujenzi wa miunndombinu hiyo kwenye bonde hilo la Cheju ‘B’ lenye ukubwa wa hekta 301 linalotarajiwa kuzinduliwa wakati wa sherehe za Mapinduzi baadae mwakani.
Wakati huo huo Mhe. shamata alitembelea na kukagua ujenzi unaoendelea wa maabara za Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Zanzibar (ZALIRI) unaotekelezwa na Kampuni ya Kin Inverstiment pamoja na kukagua ujenzi wa mradi wa Zipline unaosimamiwa na kampuni ya Eco Tourism huko Mwera Masingini, wilaya ya Magharibi ‘A’ Unguja.