
KATIBU SEIF ATOA WITO KWA TAASISI ZA SERIKALI NA BINAFSI KUSHIRIKIANA KATIKA UDHIBITI WA SUMUKUVU KWENYE SEKTA YA KILIMO.Posted: 2023-08-28
Katibu Mkuu wizara ya kilimo, Umwangiliaji, Maliasili na Mifugo Seif Shaaban Mwinyi ametoa wito kwa Taasisi za Serekali na Binafsi kushirikiana katika Udhibiti wa Sumukuvu kwenye Sekta ya Kilimo, Mifugo, Afya na Biashara ili kuweza kuwa na nguvu na Mpango utakaotuhakikishia usalama wa mifumo ya chakula. Hayo aliyasema wakati wa ufunguzi wa Semina ya kujenga uelewa kwa Wakurugenzi na Wadau kutoka Taasisi za Serikali na Binafsi iliyofanyika katika Hotel ya Ocean View iliyopo Kilimani Zanzibar. Amesema Zanzibar bado ina fursa nzuri katika kufikia malengo chanya kwenye udhibiti wa sumukuvu na kuwa na uhakika wa vyakula vilivyo salama. Hivyo, ushiriki wa wadau katika kutoa maoni yatakayosaidia kupunguza tatizo la sumukuvu nchini ni jambo la muhimu ili kudhibiti athari zisiwafikie walaji na kuwa na jamii yenye afya bora.
Nae Meneja wa Mradi wa TANiPAC kwa upande wa Zanzibar Ndugu Mwanaidi Ali khatib amesema lengo la semina hiyo ni kuwasilisha ripoti ya hali ya sumukuvu nchini na kuwa na mpango utakaoweza kudhibiti tatizo la sumukuvu katika mifumo ya chakula kuanzia kwa Mkulima hadi kwa Mlaji. Aidha, amesema mradi huu wa Udhibiti Sumukuvu ni wa miaka mitano na unaendelea kutoa elimu na namna ya udhibiti kwa Wakulima, Wajasiriamali, Mabwana shamba, Wataalamu wa Afya pamoja na kuzijengea uwezo Tasisi ya Viwango (ZBS) na Mamlaka ya Chakula na Vipodozi (ZFDA) kwa kuwapatia Mashine za kisasa za kupimia Sumukuvu.
Akiwasilisha mada katika Semina hiyo Muhadhiri kutoka Tanzania Bara Dkt. Happy Magoha amesema tatizo la sumukuvu lipo katika nchi zenye hali ya hewa ya joto duniani ambayo husababisha madhara yakiwemo Maradhi ya saratani ya ini, kupunguza kinga ya mwili na vifo kwa wanadamu kutokana na ulaji wa vyakula vilivyochafuliwa na sumukuvu zikiwemo Njugu (Karanga) na Mahindi.
Akichangia Mada Mkurugenzi kutoka Tasisi ya Utafiti wa Afya Zanzibar Khamis Rashid Kheir ameshukuru kupatiwa mafunzo hayo muhimu kwa afya za wanadamu na wanyama na kutaka Mradi wa Sumukuvu kuendelea na mafunzo kwa ngazi za Shehia ambapo zipo jamii za wakulima na wafugaji wasioelewa madhara ya sumukuvu na kutoa ushauri wa kufanyiwa vipimo vyakula vya nafaka kabla ya kuingizwa nchini Mafunzo hayo ya siku moja yameandaliwa na Mradi wa TANIPAC Tanzania