
RAIS DK.MWINYI AHIMIZA MAPINDUZI YA KILIMO ZANZIBARPosted: 2023-08-04
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi amesema lengo la Maonesho ya Kilimo ni kuhimiza kufanya Mapinduzi kwa kuelimisha juu ya umuhimu wa mbinu bora za kilimo ikiwemo matumizi ya teknolojia ya umwagiliaji maji, zana za kisasa kwa madhumuni ya kuongeza uzalishaji kwa mazao ya chakula na biashara ili kupata tija zaidi na kuwapa faida kubwa wakulima na Taifa kwa ujumla.
Ameyasema hayo akifungua Maonesho ya Kilimo ya Nane Nane yanayofanyika Kizimbani Dole Mkoa wa Mjini Magharibi, wakati akitembelea mabanda ya Taasisi za Serikali, binafsi na wajasiriamali. Aidha, Rais Dk.Mwinyi amewataka Vijana watumie fursa ya kuwepo Maonesho haya kwa kujifunza ili wahamasike kujiajiri katika sekta ya kilimo, wawe na uhakika wa uzalishaji wa chakula pamoja na maendeleo yao.
Vilevile, Rais Dk.Mwinyi amesema Serikali ina wajibu wa kuwawezesha Wakulima na itatoa fedha kwa ajili ya Pembejeo pia itaendelea kuwakaribisha wawekezaji katika sekta ya Kilimo na Ufugaji ili iweze kuongeza mchango katika pato la Taifa na kuhakikisha usalama wa chakula.