UTAMBULISHO WA MRADI WA KUJENGA UWEZO WA KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIANCHI KATIKA SEKTA YA KILIMO-February 2019

Mradi wa Kujenga Uwezo wa kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia mbinu za Kilimo Himilivu ni mradi ulioanzishwa kwa pamoja kati ya Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi - Zanzibar na Wizara ya Kilimo ya Tanzania kwa upande wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirkiana na Shirika la USAID la Marekani ambalo linasaidia kifedha. Katika utekelezaji wake Wizara hizi mbili zinashirikiana kwa pamoja na mashirika ya kimataifa ya IITA, ICRAF na FAO ambayo yamepewa majukumu kwa kila mmoja katika utekelezaji wa vipengele vya mradi na majukumu yake. Katika kuutambulisha mradi huu ili kujenga uelewa wa mradi na utekelezaji wake katika maeneo yake ya utekelezaji, kwa upande wa Wizara ya Kilimo, watendaji wakuu wa Wizara na taasisi zake, maafisa wakuu na watendaji wengine wakiwemo wanahabari walishiriki. Kwa upande wa Halmashauri za Wilaya, zilijumuishwa Wilaya ya Kusini na Kaskazini B kwa Unguja na wilaya Wete na Chakechake kwa Pemba, mikutano ya utambulisho ilihuduriwa na kuongozwa na Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala, Wakurugenzi wa Halmashauri, maafisa wa kilimo na mifugo, wanahabari, wakulima pamoja na wadau wengine. Mradi huu umegawika katika vipengele vitano ambapo kipengele cha kwanza kinahusiana na masuala ya tafiti ambacho kinatekelezwa na ICRAF,wakati kipengele cha 2,3 na 4 kinahusiana na masuala ya Uchaguzi wa teknolojia, uanzishaji wa mashamba ya maonesho pamoja na utoaji wa mafunzo kinatekelezwa na IITA na kipengele cha 5 kinashughulikia masuala ya taarifa za hali ya hewa kinatekelezwa na Shirika la Chakula Duniani (FAO) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hali ya Hewa - Tanzania (TMA) kwa lengo la kuimarisha na kuendeleza kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabianchi . Wizara za Kilimo ndio zenye majukumu ya kuhakikisha kwamba mradi unatekelezwa katika maeneo yaliyochaguliwa katika halmashauri za wilaya na zinatekeleza kilimo hiki na kuwajengea uwezo wadau wa mradi wakiwemo wakulima pamoja na maafisa wa kilimo na Serikali za mitaa katika maeneo husika pamoja na kutoa ushauri wa kitaalamu kulingana na mipango na mikakati ya kitaifa iliyowekwa. Vile vile,Wizara hizi mbili kwa kushirikiana na baadhi ya vyuo vya kilimo pamoja taasisi za utafiti zinafanya kazi ili kuendeleza kilimo pamoja na teknolojia za kilimo himilivu kwa walengwa.