UZINDUZI MPUNGA KIBOKWA-July 2018

Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Mhe. Rashid Ali Juma amesema katika jitihada za kuimarisha kilimo cha mpunga serikali imekuwa ikifanya juhudi za kuongeza uzalishaji kwa mkulima ikiwemo mbinu ya kilimo shadidi. Mhe. Waziri Amewataka wakulima wa kilimo hicho kutumia teknologia ili kuweza kupata mafanikio zaidi ya uzalishaji. Hayo ameyaeleza huko bonde la Kibokwa Wilaya Kaskazini “A” katika uzinduzi wa uvunaji wa mpunga kwa msimu wa mwaka huu na kuongeza kipato kwa wakulima. Mhe. Waziri amesema serikali ina mpango wa kujenga hekta 193 za miundombinu ya umwamgiliaji maji kupitia mradi wa kuongeza uzalishaji wa mpunga (ERPP) na lengo la serikali ni kujitosheleza kwa mchele kutoka asilimia 39.7 ya sasa hadi asilimia 60 ifikapo mwaka 2020. Nae Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Maryam Juma Abdulla amesema kilimo shadidi kimekuwa ni mkombozi kwa wakulima wa zao la mpunga kwani matunda yake yameanza kuonekana. Katibu Maryam ameeleza kuwa jumla ya tani 45,000/ za mpunga zinatarajiwa kuvunwa katika msimu huu kutoka tani 20.603 kwa miaka mitano iliyopita. Katika uzinduzi huo Mhe. Waziri Rashid alikabidhi mashine 2 za kuvunia mpunga ambazo zitatumika katika kazi za uvunaji wa mpunga.