ZIARA YA WAKULIMA WA KILIMO CHA MPUNGA MOROGORO-August 2017

Wakulima wa zao la mpunga kutoka visiwa vya Unguja na Pemba wamejionea na kupata maelezo mbali mbali juu ya kilimo cha kisasa kinachotumia mbinu mpya ijulikanayo kama kilimo shadidi. Hayo wameyapata walipotembelea katika viwanja vya maonesho ya nane nane huko Morogogro Tanzania bara. Ziara hiyo iliyoandaliwa na Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi kwa kupitia mradi wake wa Kuongeza Uzalishaji na Tija katika zao la mpunga (ERPP). Tangu kuanzishwa kwa mradi huu kila ifikapo siku ya tarehe nane mwezi wa nane ya kila mwaka, mradi huchukua wakulima wapatao ishirini, kumi kwa upande wa Unguja na kumi kwa upande wa Pemba kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa vitendo na kujionea hali halisi ya kilimo cha mpunga kwa upande wa Tanzania bara. Kila ifikapo tarehe nane ya mwezi wa nane ya kila mwaka Tanzania inaadhimisha siku ya wakulima ambayo hufanyika mikoa mbali mbali kwa lengo la kutoa taaluma kwa wakulima na wafanya biashara.